Tarehe 9 Machi, 2023, Mheshimiwa Dkt. George Vella, Rais wa Jamhuri ya Malta alipokea Hati za Utambulisho za Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo mwenye makazi yake Roma, Italia. Tukio hili muhimu na la kihistoria lilifanyika katika Ikulu ya Malta na kufuatiwa na mazungumzo ya pande mbili yaliayokisi kuimarisha ushirikiano zaidi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa na azma ya nchi ya Malta kuwa daraja baina ya Afrika na Umoja wa Ulaya. Katika mazungumzo yao, suala lililosisitizwa ni kuibua fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili katika maeneo ya elimu, utalii, utamaduni, uvuvi, usafiri wa majini, biashara na uwekezaji. Mara baada ya mazungumzo, kuliandaliwa gwaride maalum la heshima kwa ajili ya Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo. 

Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Malta ulianza mwaka 2015 na tangu wakati huo, juhudi za kukuza uhusiano huo zimekuwa zikifanyika kupitia sekta za elimu, utalii na usafiri wa anga; na kupitia katika majukwaa ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola ambazo nchi zote mbili ni wanachama. 

Katika hafla hiyo, Balozi Kombo aliambatana na Mama Zakia Kombo, mwenza wake, na Bw. Sigfried Nnembuka, Afisa Ubalozi.