Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limeupatia utambuzi rasmi Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italia kama Kituo cha Lugha na Utamaduni. Utambuzi huu ni kufuatia Ubalozi kutunikiwa Cheti cha Usajili na Dkt. Fatma Mlaki, Mchunguzi Lugha Mkuu kutoka BAKITA tarehe 28 Aprili, 2023. 

Sanjari na hayo, tukio hili lilitanguliwa na siku tano za mafunzo maalum ya stadi za kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni yaliyoanza tarehe 24 hadi 28 Aprili, 2023. Mafunzo haya yalikutanisha walimu na wahadhiri wa lugha ya Kiswahili waliopo hapa Italia pamoja na Diaspora kwa ujumla na kutunukiwa vyeti. Kupitia mafunzo hayo washiriki walipata kufahamu kwa undani stadi za kufundisha Kiswahili zinazotokana na Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji Kiswahili kwa Wageni wa mwaka 2020. 

Hatua hii chanya inalenga kutekeleza sera ya nchi ya kubidhaisha lugha ya Kiswahili sehemu mbalimbali duniani ikiwemo hapa Italia na maeneo mengine yanayowakilishwa kupitia Ubalozi huu.