Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italia na Mwakilishi wa Kudumu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Roma alishiriki Mkutano wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization) uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania, Tarehe 3–6 Februari 2026.
Pembezoni mwa mkutano huo, Balozi alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Daniel Chongolo, Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Katika mazungumzo hayo, Balozi Mbarouk aliwaeleza viongozi hao wa Wizara ya Kilimo kuwa Tanzania ni Mwenyekiti wa Kundi la Kanda ya Afrika kwa mwaka 2o26, hivyo ina jukumu kubwa la kuratibu masuala yote ya Kanda ya Afrika yanayohusu Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Roma, ambayo ni FAO, IFAD na WFP.
Aidha, Balozi Mbarouk aliwaarifu kuwa kuanzia tarehe 13 hadi 17 Aprili 2026, kutafanyika Mkutano wa FAO wa Kanda ya Afrika nchini Mauritania, mkutano ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili. Tanzania kama Mwenyekiti wa Kanda itashirikiana na Ofisi ya FAO ya Kanda ya Afrika kwenye uratibu wa mkutano huo. Balozi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na ushiriki wa wizara zote zinazohusika na sekta ya kilimo katika maandalizi na utekelezaji wa masuala yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo.
Vilevile, Balozi Mbarouk aligusia umuhimu wa Serikali kuendelea kuchangia ada za uanachama katika Mashirika ya FAO na IFAD.
