Tarehe 6 Machi, 2022 Ubalozi wa Tanzania uliopo Roma, Italia ulifanya Mkutano Mkuu wa Watanzania wanaoishi maeneo mbalimbali nchini Italia (Diaspora). Mkutano huo ulifanyika chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia na kuhudhuriwa na Wanadiaspora takriban 100 akiwemo Mhashamu Baba Askofu Mkuu Protase Rugambwa, Katibu Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. 

Mkutano huo uliofanyika kwa mafanikio ulilenga kuukutanisha Ubalozi na Jumuiya mbalimbali za Watanzania nchini Italia kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya pande mbili. Sanjari na hilo, mkutano huo ulijadili masuala mbalimbali yanayowahusu Wanadiaspora ikiwemo changamoto za kiutendaji na ushirikiano katika Jumuiya zao ambazo zilianishwa wazi kwenye taarifa za kiutendaji zilizowasilishwa na Viongozi wa Jumuiya.  Kwa nchini Italia zipo Jumuiya sita zinazotoka maeneo ya Roma, Napoli, Modena Central North, Genova, Modena na Umoja wa Watanzania Wakatoliki unaojumuisha Waklero, Watawa, Waseminari na walelewa wa Utawa wanaofanya kazi za kitume hapa Italia. 

Mkutano uliazimia kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya Wanadiaspora na Ubalozi kwa kuanisha mkakati thabiti wa kuboresha mawasiliano baina ya pande mbili. Aidha, Ubalozi kama mlezi wa Wanadiaspora hao utazitembelea Jumuiya hizo kwa ajili ya kusaidia kuwasimamia katika uchaguzi wa viongozi, kuandaa au kuboresha Katiba za Jumuiya na kutafuta suluhu ya kudumu dhidi ya changamoto wanazokabiliana nazo. 

Kwa kipekee, Mheshimiwa Balozi Kombo alitoa wito kwa Watanzania hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuiletea Tanzania maendeleo. Vilevile, aliwahimiza kujisajili katika daftari la Diaspora wa Italia ili kuwa na takwimu na kumbukumbu sahihi za Watanzania waliopo Italia. Takwimu na kumbukumbu hizi zitasaidia Ubalozi kuwaunganisha Wanadiaspora na wabia wa maendeleo ambao wana nia au tayari wanaendesha shughuli zao nchini Tanzania na wanahitaji kushirikiana na Diaspora. 

  • Mheshimiwa Balozi Kombo akipokea picha ya nembo rasmi ya Jumuiya ya Watanzania Genova kutoka kwa Bi. Eva Nangela, Mwenyekiti wa Jumuiya (kushoto).Mheshimiwa Balozi Kombo akipokea picha ya nembo rasmi ya Jumuiya ya Watanzania Genova kutoka kwa Bi. Eva Nangela, Mwenyekiti wa Jumuiya (kushoto).