Mheshimiwa Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Malta, mwenye makazi jijini Roma, Italia, amewasilisha hati za utambulisho kwa Mheshimiwa Myriam Spiteri Debono, Rais wa Jamhuri ya Malta, katika Ikulu ya Malta iliyopo jijini Valletta, tarehe 28 Oktoba 2026.

Mara baada ya kuwasilisha hati hizo, Mheshimiwa Balozi Mbarouk alifanya mazungumzo mafupi na Mheshimiwa Rais Debono, ambapo alitumia fursa hiyo kueleza nia ya Serikali ya Tanzania kuimarisha na kukuza uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Mbarouk alieleza maeneo ya kipaumbele katika ushirikiano kati ya Tanzania na Malta, hususani katika sekta za utalii, usafiri wa majini na bandari, biashara na elimu.

Aidha, alieleza dhamira yake ya kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Malta kupitia taasisi zake mbalimbali pamoja na wadau muhimu nchini humo, kwa lengo la kukuza ushirikiano katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Rais Debono alimpongeza Balozi Mbarouk kwa kuteuliwa kwake na kusisitiza umuhimu wa mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Malta ili kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili. Vilevile, Mhe. Rais Debono alieleza kuhusu uzoefu wa Malta katika sekta ya utalii na usafirishaji wa majini kuwa ni wa muda mrefu na Serikali yake ipo tayari kufungua milango ya ushirikiano na Tanzania katika sekta hizo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mhe. Rais Debono alimtakia Balozi Mbarouk heri na mafanikio katika kutekeleza majukumu yake mapya nchini Malta, huku akiahidi kumpa ushirikiano katika kipindi chake cha uwakilishi.